Friday, August 14, 2009

"Mawe ya ajabu" - Stonehenge - Wiltshire,

Ni kivutio kikubwa cha watalii hapa wingereza. Usijiulize kuangalia mawe tuuuuuu........ Soma zaidi.

Ni nguzo za mawe ambayo yalipangwa kwa mtindo wa kiduara hapo kale. Inasadikika nguzo hizo zilipangwa kati ya mwaka 3000 na 1600 kabla ya kuzaliwa Kristo. Mawe hayo yamepangwa kufuatana na machweyo na mawiyo ya jua wakati wa "kiangazi" (summer solstice) na wakati wa "baridi" (winter solstice). Siku hizi ni siku ambazo jua hufikia kilele chake "kwa kupanda" kuelekea kaskazini mwa dunia - summer solstice tarehe 21 Juni na hushuka kufikia kilele kusini mwa dunia - winter solstice Disemba 22).Pia haijulikani haswa ni akina nani walihusika kati ujenzi huo. Kwa sasa inaaminika ni "watawa" walioitwa Druids ndio waliosimamisha nguzo hizo. Mawe kwaajili ya Stonehenge yalitoka mbali kama maili 200. Kufika kwenye eneo hilo (kwa kuwa hapakuwa na malori) walitumia njia ya kuyavuta juu ya miti na ilihitaji watu wengi kufanikisha zoezi hilo.

Kazi ya kuyasimamisha pia haikuwa rahisi. Watu hawa walikuwa na akili za ajabu za kufikiria nyenzo ya kuwezesha mawe haya ambapo jiwe zito kabisa lilikuwa na uzito wa tani 26 kusimamishwa. Theluthi moja ya jiwe iko chini ya ardhi.

Dhumuni halisi ya mawe hayo mpaka sasa haijulikani vizuri. Pamekuwa na nadharia nyingi zikiwamo za kidini na za kiunajimu. Kidini sehemu hiyo ilikuwa ya kuabudia na kutoa kafara ikiwemo ya binadamu.


Mawe haya mpaka leo yanatumika na baadhi ya watu kuambudia.

Kiunajimu, wakati wa "summer solstice" miale ya jua la asubuhi hupitia katikati ya mawe yaitwayo "Heel stones" na miale hiyo hufika moja kwa moja kwenye jiwe liitwalo Alter stone". Hii pia inawezekana ilikuwa njia moja wapo ya kutambua majira ya mwaka.

Mawe haya pia kunauwezekano yalitumika kujua na kutunza rekodi (kwa kadiri ya miaka 20) za mambo ya angani usiku kama kupatwa kwa mwezi. Mpango wa mawe hayo husaidia kujua kupatwa kwa mwezi.

Kwa kuwa hakuna nyaraka zozote zilizo achwa kimaandishi au kipicha achilia mbali kisauti, mpaka leo wanasayansi wanajaribu kuunganisha nadharia zao tuu ili kujua haswa kwa nini nguzo hizo zilisimamishwa, na kwa nini walijituma kutafuta mawe makubwa kiasi hicho hata kwa umbali wa maili 200, Je, ilikuwa kwaajili ya kuabudu tuu au kujua majira ya mwaka na mambo yatokeavyoo mbinguni usiku tuu. Kuna nadharia nyingi ambazo siwezi kuweka zote kwenye blogu hii. Ila ni matumaini yangu kuwa umepata kajimwanga kidogo kuhusu mawe haya ya ajabu.

soma pia: http://www.english-heritage.org.uk/server/show/nav.16470

No comments: